CHADEMA yapongeza matumizi ya usaili kupata wakuu wa mashirika umma

0
16

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mrema amesema uamuzi wa serikali kutaka kubadili utaratibu wa kuwapata watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma, kuanza kutumia njia ya usaili ni jambo jema endapo litatekelezwa.

Ameyasema hayo baada ya Serikali kuweka wazi juu ya wakuu wa mashirika ya umma na wajumbe wa bodi kufanyiwa usaili ili kuongeza tija kwenye taasisi husika, na kupunguza utegemezi wake serikalini kujiendesha ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa kodi.

“Hiyo inaleta ufanisi kwa sababu mtu anajua kwamba hiyo kazi hajapendelewa, hateuliwi kwa sababu ya ukada au ukaribu na mamlaka ya uteuzi, bali kwa sababu ya sifa na weledi alionao,” amesema Mrema.

Ameongeza kuwa ‘huo ndiyo umuhimu wa katiba mpya, pawekwe utaratibu wa watu kuomba hizo kazi kwa sababu mtu anaweza kuteuliwa wakati hana hata nia ya kuomba hiyo kazi.”

Aidha Mrema ameshauri jambo hilo lisiishie kwenye mashirika ya umma pekee bali lifikie hadi kwenye taasisi nyeti za umma.

Naye mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza amesema hilo ni jambo zuri, lakini anatamani kujua litatekelezwa katika mfumo gani, kwa sababu amedai kuwa unaweza kufanya usaili lakini usiwe na utaratibu ambao ni wazi na huru.

Send this to a friend