CHADEMA yashtushwa Sumaye kutumia nembo ya taifa kuitisha mkutano wa wanahabari

0
13

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kimeshtushwa kuona mwanachama wake ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye akitumia nembo ya taifa katika barua yake ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari unaotarajiwa kufanyika leo katika jengo la LAPF, lililopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi  Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema amesema kuwa chama hicho hakina taarifa za mkutano huo na kwamba wameona barua hiyo mitandaoni kama ilivyokuwa kwa wananchi wengine.

Tunaona barua hiyo katika mitandao kama wengine, tumeshtushwa kuona barua yenye nembo ya Taifa inatumika kuitisha mkutano wa kiongozi wetu.

Sumaye anatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari leo, mkutano ambao umeitishwa siku chache baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani, ambapo licha ya kuwa mgombea pekee, alipata kura 48 za hapana kati ya kura 76 zilizopigwa.

Watu wakiendelea kujiuliza kiongozi huyo atazungumza nini, barua ya kuitisha mkutano huo imeeleza kuwa lengo la mkutano huo ni kuzungumzia masuala ya siasa nchini na mwenendo wa uchaguzi wa CHADEMA unaoendelea.

Amekuwa mwanachama wa CHADEMA kwa zaidi ya miaka minne sasa, ambapo alijiunga Agosti 2015 wakati wa harakati cha uchaguzi mkuu.

Kiongozi huyo pia amechukua fomu ya kugombea uenyekiti wa CHADEMA Taifa, huku akisema kuwa lengo la kuchukua fomu hiyo ni kuuonesha ulimwengu kuwa ndani ya CHADEMA kuna Demokrasia, na sio kweli kwamba nafasi ya mwenyekiti haiguswi.

Send this to a friend