
Kufuatia madai ya aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Mohamed, kwamba amefungua kesi kwa niaba ya chama hicho kuhusu mgawanyo wa mali, CHADEMA Zanzibar imesema kesi hiyo ni yake binafsi pamoja na watu wanaomshawishi au kumtuma.
Chama hicho kimefafanua kuwa Said Mohamed hana nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama na kwamba kauli zake hazina uhalali, hivyo wananchi wanapaswa kupuuza taarifa hizo zinazodaiwa kupotosha umma.
“Kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za CHADEMA, yeye ni mwanachama wa kawaida asiye na mamlaka ya kuzungumza, kuamua au kuchukua hatua yoyote kwa niaba ya CHADEMA Zanzibar,” imesema taarifa iliyotolewa na CHADEMA Zanzibar.
Aidha, imeongeza masuala yote yanayohusu umiliki, usimamizi na mgawanyo wa mali za CHADEMA Zanzibar hushughulikiwa na vyombo halali vya chama kwa mujibu wa Katiba na Kanuni na taratibu zake, na si kwa matakwa ya mtu binafsi.







