Chama cha Marubani chasema marubani hujiongoza wenyewe kutua Bukoba

0
12

Katibu wa Chama cha Marubani Tanzania (TAPA), Kapteni Khalil Iqbal amesema kuna baadhi ya makampuni ya ndege ambayo yanawashinikiza marubani kufanya safari zao katika mazingira hatarishi hali inayohatarisha usalama wa abiria na wafanyakazi.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha habari cha Azam TV kuhusu ndege ya ATCL kushindwa kutua Uwanja wa Bukoba, Kagera, Kapteni Iqbal amesema baadhi ya marubani wamekuwa wakitoa malalamiko yao kwenye chama na malalamiko hayo kupelekwa kwenye Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) lakini hakuna chochote kinachofanyika na badala yake hufukuzwa kazi.

“ Kuna fununu tumepokea kwamba kuna ‘memo’ zimetoka kwenye mashirika mbalimbali memo kwa marubani, kuna rubani amekatwa mshahara kwa kutokwenda pale [mahali hatari], kuna rubani amefukuzwa kazi kwa sababu amelalamika mataa,” ameeleza Kapteni Iqbal.

Aidha, amefafanua kuwa katika uwanja wa ndege wa Bukoba hakuna mwongozaji wa ndege ambaye anawaongoza marubani, badala yake marubani hujiongoza wenyewe.

Amesema rubani wa ndege anapokuwa umbali wa maili 30 (takribani 100km) kufika Uwanja wa Ndege wa Bukoba, mwongozaji wa ndege kutoka Mwanza humwacha, na hivyo rubani huwasiliana na mtumishi mwenzi aliye uwanjani ambaye humweleza hali ya uwanja, lakini suala lote la kutua, ni rubani hujiongoza.

Amewapongeza marubani wa ATCL kuamua kurejea Mwanza baada ya ndege kushindwa kutua Bukoba, akisema uamuzi huo ni wa kitaalamu, japo nyakati nyingine marubani ambao hukataa kutua hukumbana na kadhia ikiwa ni pamoja na kukatwa mishahara au kufukuzwa kazi.

Send this to a friend