
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima, amesema kuwa chama chochote cha siasa ambacho hakitasaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi hapo kesho Aprili 12, 2025, hakitapata nafasi ya kusimamisha mgombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza na Azam TV, Kailima ameeleza kuwa mgombea wa chama ambacho hakitasaini maadili hayo hatakuwa na fursa ya kujaza fomu namba 10 wakati wa kuwasilisha fomu za uteuzi. Hii ni kwa sababu chama chake kitakuwa hakijakubaliana rasmi na maadili hayo, ambayo ni sehemu muhimu ya mchakato wa uchaguzi.
“Chama cha siasa ambacho hakitasaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi kesho, hakitapata fursa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu. Maadili haya yanapaswa kusainiwa na kuzingatiwa na chama cha siasa, mgombea, tume, na Serikali,” alisema Kailima.
Aidha, amebainisha kuwa mpaka sasa hakuna chama chochote cha siasa kilichowasilisha malalamiko kuhusu kanuni hizo, hivyo mchakato wa kusaini na kuzizingatia unatarajiwa kuendelea kama ilivyopangwa.