Chanjo na kodi vyawafikisha Askofu Gwajima na Silaa kamati ya maadili

0
41

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameamuru wabunge Josephat Gwajima (Kawe) na Jerry Silaa (Ukonga) kupelekwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kujibu tuhuma mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo kusema uongo na kushusha hadhi na heshima ya bunge.

Ndugai ameagiza Gwajima ambaye ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kufika mbele ya kamati Agosti 23 mwaka huu, na Silaa kufika mbele ya kamati siku inayofuata (Agosti 24).

Licha ya kuwa taarifa ya bunge haijaeleza makosa ambayo wawili hao wanatuhumiwa kwayo, lakini kwa siku za hivi karibuni Askofu Gwajima amekuwa akidai kuwa chanjo ya UVIKO-19 ambayo imeanza kutolewa nchi haujulikani kama ni salama au la kwa sababu hakuna uchunguzi wa kina uliofanyika juu ya madhara yake kwa binadamu, hivyo kuhumuza wananchi wasichanjwe.

Agosti 17, 2021 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima aliamuru mbunge huyo akamatwe ili athibitishe shutuma alizotoa dhidi yake na Rais wa Tanzania kuwa wamepokea hongo ili kuingiza chanjo za UVIKO-19 nchini.

Waziri alisema Askofu Gwajima anaivuruga wizara yake na serikali kwa ujumla hasa katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa kutoa taarifa za kupotosha juu ya chanjo na hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yake, jambo ambalo limekuwa likileta mkanganyiko katika jamii na kwamba sasa umefika mwisho wa upotoshaji huo.

Kwa upande wa Silaa, huenda ameitwa mbele ya kamati kufuatia kusema kuwa wabunge hawakwatwi kodi ya malipo, na hivyo kutaka hilo kufanyika ili kuongeza mapato ya serikali.

“Ni wakati muafaka sisi waheshimiwa wabunge ili tupate uwezo wa kuwaambia Watu waanze kulipa kodi na sisi tuanze kulipa kodi katika mishahara yetu, hakuna sababu ya kuwa wengine wanalipa wengine hawalipi ukishakuwa haulipi unakosa ile nguvu ya kumwambia mwenzako alipe,” alisema Silaa katika mkutano wa hadhara jimboni kwake.

Hata hivyo bunge lilikanusha taarifa hiyo na kusema kuwa wabunge kama ilivyo kwa viongozi na watumishi wengine, wanalipa kodi zote kwa mujibu wa sheria ikiwemo kodi ya mapato (PAYE).

Taarifa ya Bunge imeonya kuwa endapo Gwajima na Silaa hawatofika mbele ya kamati kwa muda unaotakiwa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Send this to a friend