China: Mwandishi ahukumiwa jela miaka 4 kwa kuripoti kuhusu corona Wuhan

0
25

Mahakama nchini China imemhukumu kifungo cha miaka minne jela mwandishi wa habari wa kujitegemea baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuhatarisha amani na uchochezi.

Zhang Zhan ametiwa hatiani kwa makosa hayo baada ya kuripoti hali ilivyo mjini Wuhan kufuatia mlipuko wa virusi vya corona mjini humo.

Mwanasheria huyo wa zamani mwenye miaka 37 ni miongoni mwa waandishi wa kujitegemea ambapo wamekumbana na mkono wa dola kwa kuripoti matukio kutokea Wuhan.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mwandishi huyo alifika Wuhan Februari kuripoti kuhusu virusi hivyo, ripoti zake na matangazo mbashara yalisambazwa kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii, na hivyo kuzishtua mamlaka za serikali.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu China (CHRD) umesema kuwa Zhan alijikita kuonesha namna waandishi wengine wa kujitegemea na familia za waathirika zilizvyokuwa zikinyanyaswa.

CHRD imesema kuwa Mei 14 Zhan alipotea na siku moja baadaye aliripotiwa kuwa anashikiliwa na polisi mjini Shanghai, umbali wa 640km kutoka alipokuwa mara ya mwisho.

Alishtakiwa Novemba 2020 akidaiwa kusambaza taarifa za uongo kupitia WeChat, Twitter na YouTube. Pia, alishitakiwa kwa kukubali kufanya mahojiano na vyombo vya habari vya nje na kusambaza taarifa za uongo.

Upande wa mashitaka uliiomba mahakama kumpa adhabu ya kifungo cha kati ya miaka minne na mitano.

Send this to a friend