
Rais wa China, Xi Jinping, amesema taifa lake limeendelea kwa zaidi ya miaka 70 kwa kutegemea juhudi zake binafsi na si msaada kutoka nje, huku akisisitiza kuwa nchi yake haihofii ushuru mkubwa uliowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Akizungumza na Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez, Jinping amesema hakuna mshindi katika vita vya kibiashara, na kwenda kinyume na dunia kutasababisha kujitenga tu.
“Bila kujali jinsi mazingira ya nje yanavyobadilika, China itaendelea kuwa na imani, kujikita kwenye malengo yake, na kuzingatia kusimamia mambo yake vizuri,” amesema.
Mvutano wa kibiashara umeongezeka baada ya Rais Trump kuongeza ushuru kwa bidhaa za China hadi asilimia 125, hatua iliyosababisha China kujibu kwa kuweka ushuru wa asilimia 84 na kuzuia baadhi ya kampuni za Marekani kufanya biashara nchini humo.