China yaahidi kufadhili zaidi ya trilioni 137 barani Afrika

0
72

Rais wa China Xi Jinping ameahidi kutoa zaidi ya $50 bilioni [TZS trilioni 136] katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa ajili ya kufadhili maendeleo barani Afrika.

Akiwahutubia viongozi wa Afrika katika mkutano mkubwa wa China na Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Great Hall of the People jijini Beijing, tangu kuanza kwa janga la UVIKO-19, Xi amesema lengo la msaada huo ni kuimarisha ushirikiano katika miundombinu, biashara, na sekta za kilimo, madini, na nishati.

“China iko tayari kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika katika sekta ya viwanda, kilimo, miundombinu, biashara na uwekezaji. Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, serikali ya China iko tayari kutoa msaada wa kifedha unaofikia yuan bilioni 360 [TZS trilioni 137],” amesema Rais Xi.

Amesema zaidi ya nusu ya kiasi hicho kitakuwa katika mikopo, huku akieleza kuwa $11 bilioni [TZS trilioni 29.9] zitakuwa katika aina mbalimbali za msaada pamoja na $10 bilioni [TZS trilioni 27.1] kupitia kuhamasisha makampuni ya Kichina kuwekeza.

Mbali na hayo, Xi Jinping ameahidi kuwa China itasaidia kuunda ajira milioni moja barani Afrika.

Katika mkutano huo, zaidi ya viongozi 50 wa Afrika akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wamehudhuria.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Guterres amesema uhusiano wa karibu kati ya China na Afrika unaweza kusaidia kuendesha mapinduzi ya nishati mbadala, akitoa mfano wa rekodi ya maendeleo ya China ikiwa ni pamoja na kutokomeza umasikini.

Send this to a friend