Chongolo aipa TBS siku saba kukipa ithibati kiwanda cha Masoud Kipanya

0
21

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametoa siku saba kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS)  kufika katika kiwanda cha uzalishaji magari cha Alli Masoud maarufu Masoud Kipanya ili kufanya ukaguzi na kutoa vibali vinavyohitajika ili kuruhusu uzalishaji.

Akizungumza leo  Aprili 12, 2022 Vingunguti jijini Dar es Salaam alipotembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda hicho, Chongolo ameeleza kuwa akiwa kama mtendaji mkuu wa CCM atahakikisha wanathamini mchango wa wazalishaji wa ndani kikiwemo kiwanda hicho, hivyo uwezeshaji wa kiwanda hicho ni muhimu ili kuongeza ajira kwa wananchi.

“Naiagiza TBS ndani ya siku saba ije hapa ili kukamilisha taratibu za usajili na kukipatia kiwanda hati za ithibati, kwetu hili sio dogo kwa kuwa ilani imeelekeza na kutoa msukumo katika kukuza ubunifu. Nikuahidi nitakushika mkono na kufanya harambee ili wadau waunge mkono juhudi hizi ili kukujengea uwezo wa kifedha katika kukiimarisha kiwanda hiki,” amesema Chongolo.

Aidha ameahidi ndani ya siku 14 atarudi akiwa na taasisi zote zinazohusika na udhibiti wa ubora, ili kuharakisha mchakato wa kiwanda hicho unaendelea.

Hata hivyo, Chongolo amemuomba Masoud kuendeleza ubunifu huo na kumsihi kutovunjika moyo kwani chama na Serikali vipo pamoja naye.