
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi amesisitiza kuwa si sawa kwa Afrika kushurutisha nchi zilizoendelea kutoa fedha za mabadiliko ya tabianchi, kwani ni wajibu wao wa msingi katika kulinda tabianchi duniani kote.
Ameyasema hayo akimwakilisha Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango katika Mjadala uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika kuhusu Tabianchi Addis Ababa, Ethiopia ukiangazia Mahitaji ya Fedha ya Afrika ya Ufadhili wa Mabadiliko ya Tabianchi Kabla ya COP30 (Africa’s Climate Finance Demands Ahead of COP30).
“Afrika haitakaa tena pembeni na kungoja. Tunapiga hatua mbele kudai nafasi yetu stahiki katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ulimwenguni. Bara letu linastahili ufadhili wa uhakika, wa haki na wa kutosha ili kufikia suluhu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupunguza athari zake, na kuendeleza maendeleo stahimilivu kwa Afrika. Hili si suala la hisani,” amesisitiza.
Ameeleza kuwa ufinyu wa fedha ni moja ya changamoto kubwa zinazozuia kupiga hatua kubwa katika mapambano hayo. Afrika ambayo inachangia asilimia 4 tu katika uchafuzi wa hali ya hewa, inahitaji dola bilioni 61 kila mwaka kugharamia mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo kwa sasa inapokea kiasi cha chini ya asilimia 36 ya fedha hizo.
Naibu Waziri ameongeza kuwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hupokea chini ya asilimia 5 ya fedha hizo na ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi ukilinganisha na uchangiaji wake katika janga hilo.








