Citizen TV Kenya yamuomba radhi Rais Magufuli
Kituo cha Televisheni cha Citizen (Citizen TV) cha nchini Kenya kimemuomba radhi Rais John Pombe Magufuli kutokana na kutumia maneno yasiyofaa wakati kikielezea msimamo wa Tanzania katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.
Machi 22 mwaka huu kituo hicho cha habari kilitumia maneno hayo wakati kiliporusha taarifa kikielezea kauli ya Rais Magufuli aliyotoa kuwa janga la virusi vya corona lisitumike kama kigezo cha kuharibu uchumi wa Tanzania.
Aidha, katika taarifa yake iliyotoa ya kujutia kitendo hicho, Citizen TV imesema maneno yaliyotumika hayakuwa na lengo la kupotosha kuhusu msimamo wa Rais wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika juhudi za kupambana na COVID-19.
Katika mahojiano na kituo hicho, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pinda Chanda amesema kuwa Rais Magufuli amesimama kidete na Jumuiya ya Afrika Mashariki, na jumuiya ya kimataifa katika mapambano ya ugonjwa huo.
“Citizen TV hivyo basi inakiri kuwa matumizi ya maneno hayo hayakufaa,” kituo hicho kimeeleza katika taarifa yake.