Corona: CHADEMA yawaagiza wabunge wake kutohudhuria vikao vya bunge

0
43

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewataka wabunge wake kusitisha mara moja kuhudhuria vikao vya bunge pamoja na kamati zake, ili kujikinga na maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambapo amesema kutokana na Watanzania wakiwemo wabunge kuendelea kufariki, na wakati wakiendelea kusubiri wenye mamlaka kutekeleza mapendekezo waliyotoa, wameamua kuchukua tahadhari zaidi ili kunusuru maisha ya wengine.

Mbali na kuwazuia kuhudhuria vikao vya Bunge la bajeti ambalo linaendelea jijini Dodoma, Mbowe amewataka wabunge hao kujiweka karantini kwa wiki mbili au zaidi, ili wajue hali ya afya zao.

Pamoja na hilo, amewataka kutokufika katika maeneo ya bunge jijini Dodoma na Dar es Salaam, pia wasiende kwenye majimbo yao au mikoa mingine hadi hapo watakapofahamu hali za afya zao.

Chama hicho kimelishauri bunge kusitisha shughuli zote kwa siku 21 ili wabunge na watumishi waende karantini kwa siku 21, wabunge wote, watumishi na familia zao wapimwe afya zao, na shughuli nyingine zifanyike kwa njia ya mtandao.

Aidha, chama hicho kimewashauri wabunge wa vyama vingine kutafakari kama bado ni salama kuendelea na vikao vya bunge.

Send this to a friend