Corona: Naibu Waziri wa Afya asema dalili za wagonjwa nchini na nje ya nchi zinatofautiana

0
14

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ameiagiza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya utafiti kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid-19) kwa kuwa kuna tofauti kubwa ya dalili zilizojitokeza kwa wagonjwa hapa nchini ukilinganisha na wagonjwa waliopo nje ya nchi.

Dkt. Faustine Ndugulile ametoa agizo hilo alipokutana na watafiti wa taasisi hiyo wakati wakijadili masuala mbalimbali kuhusu virusi hivyo, ambapo miongoni mwa yaliyojadiliwa ni maambukizi ya ugonjwa wa Corona na matibabu ambayo wagonjwa wanatakiwa kupatiwa.

“Kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyafanyia utafiti wa kisanyansi, moja ni uelewa wa jamii, tunataka kujua wagonjwa wanaougua Corona ni wagonjwa wa namna gani, wana magonjwa ya aina gani, dalili zinazowapata wagonjwa ni za aina gani. Hapa tunataka tupate uwelewa,” amesema Dkt. Ndugulile.

Akizungumzia matumizi ya tiba asili/tiba mbadala, Ndugulile amesema “kutokana na muitikio mkubwa wa tiba asili na tiba mbadala, kupitia kikao hiki nawaelekeza wataalamu wetu wajipange kufanya utafiti na kutoa majibu ya tiba ya maambukizi ya virusi vya Corona.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya amesema mapambano dhidi ya ugonjwa Covid-19 ni vita ambayo inapaswa kufanyiwa utafiti ambao utasaidia kupatikana kwa njia sahihi za kukabiliana na maambukizi ya ugponjwa huo.

“Tunafahamu kwamba jamii za kiafrika zina utaalamu katika miti shamba. Katika hili kuna tafiti mbalimbali zinaendelea ili kuchunguza uwezo wa miti shamba kwa lengo la kupunguza makali ya Covid-19,” amesema Prof. Mgaya

Send this to a friend