Corona: Rais Magufuli asema Dar es Salaam haitofungwa (lockdown)

0
41

Rais Magufuli amesema Serikali haitawafungia wananchi majumbani (lockdown) wala kulifunga Jiji la Dar es Salaam kama ambavyo baadhi ya watu wamependekeza, ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Ameeleza kuwa hatua hiyo haitachukuliwa ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kuwakumba wananchi na kuathiri uchumi wa nchi.

Rais Magufuli amesema hayo Aprili 22, 2020 wakati akizungumza na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama akiwa Chato mkoani, Geita kuhusu hali ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Aidha, amewataka Watanzania kuondoa hofu, kuendelea kuchukua tahadhari huku wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa.

Wakati huo huo amewaagiza viongozi wakuu wa vyombo vya uinzi na usalama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaosababisha hofu kwa wananchi na kusambaza taarifa zisizo sahihi wakiwemo wanasiasa ambao amewaonya kuacha kutafuta umaarufu wa kisiasa kupitia janga hili, na badala yake Watanzania wote waungane kupambana nalo.

Send this to a friend