Mkuu wa Mkoa wa Songwe amewataka wananchi wote wa mkoani humo kuchukua tahadhari kwa kuwa kumekuwa na wageni wengi wanao ingia Songwe kutoka katika mikoa mbalimbali hasa yenye wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya corona.
Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameyasema hayo wakati akipokea mchango wa shilingi 280,000 kutoka Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, Jimbo la Magharibi (Songwe) kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19) mkoani humo.
“Kwa sasa mkoa wetu umeanza kupokea wageni wengi kutoka Dar es Salaam na hata Zanzibar, hatuwezi kuwazuia kwakuwa nchi yetu ni moja lakini tusaidiane kutoa elimu ya Corona kwa wageni hao na tuchukue tahadhari zote muhimu.” amesema Brig. Jen. Mwangela.
Ameongeza kuwa kila mwananchi akipata mgeni kutoka maenei hayo waangalie namna ya kutenga chumba kwa ajili yake ili asichangamane na watu wengine au kutoa taarifa kwa uongozi wowote endapo watakuwa na mashaka na hali ya afya ya wageni hao ili waweze kujikinga na ugonjwa wa Corona.
Kwa upande wake Mkuu wa KKKT Jimbo la Mgharibi (Songwe), Mchungaji John Mwasakilali amempongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kutofunga shughuli za ibada kwa makanisa hayo.
Mch. Mwasakilali ameongeza kuwa wamechukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya virusi vya Corona kwa kupunguza muda wa ibada hadi kufikia saa moja, kukaa kwa kuachiana nafasi na kunawa kwa maji tiririka na sabuni na kuwa waumini wake wametii maelekezo ya serikali.