Corona: Shirika la Fedha Duniani laisamehe Tanzania deni la bilioni 33
Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeisamehe Tanzania deni lenye thamani ya $14.3 milioni (TZS 33.1 bilioni) ambalo lilipaswa kulipwa ndani ya miezi minne ijayo, kuanzia Juni 10, 2020 hadi Oktoba 13, 2020.
IMF imechukua hatua hiyo kupitia mfuko wake wa Catastrophe Containment and Relief Trust (CCRT) ili kuiwezesha Tanzania kukabiliana na athari za virusi vya corona katika nyanja za kijamii na kiuchumi.
Taasisi hiyo imesema kutegemeana na uwepo wa fedha katika mfuko huo, huenda ikaongeza msamaha wa deni lenye thamani ya $11.4 milioni (TZS 26.4 bilioni) ambalo linatakiwa kulipwa kati ya Oktoba 14, 2020 na Aprili 13, 2022, hivyo kufanya jumla ya msamaha wote kufikia $25.7 milioni (TZS 59.5 bilioni).
Taarifa ya IMF imeeleza kuwa janga la corona limesababisha athari mbalimbali nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kupungua kwa watalii, changamoto za kibajeti na kupungua kwa makadirio ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) kutoka 6% hadi 4% katika mwaka huu wa fedha, na 2.8% katika mwaka wa fedha ujao.
IMF imeisisitiza Tanzania kutumia fedha hizo kwa uwazi kukabiliana na athari za homa ya mapafu (COVID-19), ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa matumizi na kuendeleaza ushirikiano Shirika la Afya Duniani (WHO), wakala wa kimataifa na wafadhili.
Hatua hii imekuja ikiwa ni takribani miezi miwili tangu Rais wa Tanzania, Dkt Magufuli alipozitaka nchi zote za Afrika kuungana kuziomba taasisi za kifedha za kimataifa ambazo zimetangaza kusaidia mataifa ya Afrika, kutoa msamaha wa madeni badala ya kutaka kukopesha mikopo mingine ilihali nchi hizo zinakabiliwa na madeni ya mikopo ya zamani.
Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya wizara ya afya nchini Tanzania, idadi ya waathirika wa Covid-19 imeendelea kupungua ambapo mikoa 15 hana mgonjwa, huku wagonjwa waliopo kwenye maeneo mengine wakiendelea vizuri.