Coronavirus Kenya: Nane watengeneza msiba feki kuikimbia Nairobi

0
18

Kundi la watu nane ambao ni waombolezaji feki wanashikiliwa na polisi nchini Kenya kwa kudanganya kuwa walikuwa wanakwenda msibani, lengo lao likiwa ni kukwepa sheria za kudhibiti virusi vya corona jijini Nairobi.

Watu hao walinunua jeneza na kuliweka juu ya gari, na waliposimamishwa na polisi walisema wanasafirisha mwili wa marehemu kwenda Homa Bay kwa ajili ya mazishi na walikuwa wakitumia kibali cha kughushi cha mazishi walichopata kutoka Hospitali ya Mama Lucy jijini Nairobi.

Hata hivyo uongo wao ulibainika baada ya majirani wa eneo walilokuwa wanakwenda kukusanyika pamoja na wasifiri hao kwa ajili ya kuomboleza, walipoomba jeneza kufunguliwa ili wauone mwili wa aliyefariki, ndipo walibaini kuwa lilikuwa tupu.

Majibu ya vipimo vya corona yameonesha kuwa dereva wa gari hilo ana maambukizi ya virusi hivyo, na sasa wengine wamewekwa karantini, huku polisi wakiendelea na uchunguzi kubaini watu waliokaribiana na wasafiri hao kutoka Nairobi hadi Homa Bay.

Mbali na watu hao kutengeneza kifo cha uongo, kumekuwepo na ripoti kutoka nchini humo kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiwapa rushwa maafisa wa serikali ili watoroke karantini, wengine wakitengeneza dharura ili waruhusiwe kutoka nje ya nyumba zao au wasafiri baada ya muda wa kuwa nje kuisha, hatua zinazoweza kupelekea maambukizi zaidi ya virusi hivyo.

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe amesema kuwa nchi hiyo yenye visa 262 hadi sasa inaweza ikapoteza watu 28,000 endapo hatua za makusudi hazitochukuliwa sasa.

Send this to a friend