Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imesema miradi ya kimkakati ya Serikali chini ya tume hiyo inalenga kuipunguzia serikali gharama mbalimbali zikiwemo za matibabu.
Hayo yameelezwa na Afisa Uhusiano wa COSTECH, Faisal Abdul kwenye ziara na Wahariri wa Vyombo vya Habari na tume hiyo iliyofanyika Oktoba 21,2023, walipotembelea miradi ya kimkakati iliyopo mkoani Dar es Salaam na Pwani.
“Kuna mbunifu yule anayevuna sumu ya nyuki anasaidia sana anasaidia sana serikali katika kupunguza gharama za matibabu ambayo inaipunguzia serikali mzigo.
“Kwahiyo anazalisha hiyo sumu ya nyuki na inatumika kama mbadala ya magonjwa yasiyoambukizwa.” amesema Faisal.
Aidha, Faisal amesema lengo kuu la tume hiyo ikiwa kama mshauri kwa serikali ni kuwawezesha na kuwainua watafiti mbalimbali nchini ili tafiti zao ziweze kuwa na tija wakati huu ambao taifa lipo kwenye mapinduzi ya viwanda na ujengaji wa uchumi shindani.