COVID19: Rais Samia ataka nchi za Afrika kusamehewa madeni

0
14

Kutokana na athari za COVID19 katika uchumi wa nchi mbalimbali hasa za Afrika, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua stahiki kuokoa uchumi wa nchi za Afrika zikiwemo mashirika ya fedha ya kimataifa kuongeza mikopo yenye masharti nafuu kwa miradi ya maendeleo ya nchi za Afrika na kusaidia sekta binafsi katika Bara la Afrika kwa kuiwezesha kupata mikopo nafuu ili kukuza biashara hasa ndogo na za kati ambazo ndio nguzo muhimu ya uchumi.

Hatua nyingine amesema ni kusamehe mikopo ama kuongeza muda wa ulipaji wa mikopo ambayo nchi za Afrika zinadaiwa na kuchangia fedha katika bajeti za nchi za Afrika kutokana na nchi hizo kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Rais ametoa wito huo leo aliposhiriki kwa njia ya mtandao mkutano wa wakuu wa nchi na mashirika ya kimataifa uliojadili namna ya kuokoa uchumi wa nchi za Afrika kufuatia madhara yaliyosababishwa na janga la ugonjwa Korona (Covid-19), mkutano uliofanyika jijini Paris kwa wito wa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Rais ameungana na marais wengine duniani kumpongeza Rais Macron kwa kuitisha mkutano huo ambao wamesema umelenga sio tu kusaidia uchumi wa bara la Afrika bali kuokoa maisha ya binadamu waliopo Afrika kutokana na kuathirika na madhara yaliyosababishwa na Korona.

Amesema Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani imekumbwa na madhara ya ugonjwa wa corona ambayo yameathiri biashara, utoaji wa huduma za kijamii, kushuka kwa mapato, kupoteza maisha na kupoteza ajira mambo ambayo yamewaathiri zaidi wanawake, vijana na watoto.

Send this to a friend