
Benki ya CRDB, ambayo ndiyo mdhamini mkuu wa Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB, imesema malipo yote ya bingwa wa msimu uliopita yalifanyika kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kama sehemu ya makubaliano ya udhamini wa mashindano.
Taarifa hiyo imejiri baada ya Afisa Habari wa Yanga SC, Ally Kamwe kuiambia TFF pamoja na benki hiyo kuwa klabu hiyo haitacheza fainali ya CRDB ikiwa haitalipwa fedha za ubingwa msimu uliopita.
“Tungependa kufahamisha umma na wadau wote wa soka kuwa Benki ya CRDB ni taasisi yenye kuzingatia weledi, kanuni na taratibu, na kwa msingi huo tayari benki ilikwisha tekeleza kikamilifu wajibu wake wa kifedha kwa TFF kama sehemu ya makubaliano ya udhamini wa mashindano haya. Malipo yote ya msimu uliopita yalifanyika kwa TFF kwa mujibu wa mkataba baina ya benki ya CRDB na TFF,” imesema taarifa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa dhamira ya benki hiyo ni kuendelea kushirikiana na TFF, vilabu na wadau wengine katika kukuza mchezo huu kwa maslahi mapana ya Taifa.
