Cristiano Ronaldo, mwanasoka wa kwanza bilionea duniani

0
15

Mshambuliaji wa Juventus ya Italia, Cristiano Ronaldo ameweka rekodi nyingine kwa kuwa mwanasoka wa kwanza bilionea duniani.

Mwaka uliopita Ronaldo aliingiza $105 milioni (TZS 243.3 bilioni) kabla ya kodi na ada nyingine, hivyo kushika nafasi ya nne kati ya mastaa 100 wa Jarida la Forbes.

Kipato hicho kimemfanya Ronaldo kuwa mchezaji soka pekee katika historia kuwahi kupata $1 bilioni (TZS 2.3 trilioni) katika muda wake wa soka.

Nyota huyo mwenye miaka 35 amekuwa mwanamichezo wa tatu kufikia hatua hiyo akiwa bado anacheza baada ya Tiger Woods mwaka 2009 na Floyd Mayweather mwaka 2017.

Ronaldo ameingiza jumla ya $650 milioni (TZS 1.4 trilioni) ndani ya uwanja katika kipindi cha miaka 17 ya soka la kulipwa, na anatarajiwa kufikia $765 milioni (TZS 1.8 trilioni) katika mshahara wake kutokana na mkataba wake wa sasa unaoishia Juni 2022.

Mapato ya nyota huyo kwa mwaka 2020 yanajumuisha mshahara wa $60 milioni (TZS 139 bilioni), kiwango hiki ni kidogo ikilinganishwa na mwaka 2019 kutokana na mchezaji huyo kuridhia kukatwa 30% kutokana na janga la corona.

Send this to a friend