CWT yampongeza Rais Samia kwa kuboresha maslahi ya Walimu

0
40

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maslahi ya walimu ikiwemo upandishwaji wa madaraja wa walimu 127,000 na kutenga kiasi cha TZS bilioni 55.57 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 809 za walimu.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 7,2022 jijini Dodoma na Kaimu Rais wa CWT, Mwalimu Dinna Mathamani wakati akizungumza na waandishi wa habari, amesema tangu Rais Samia aiingie madarakani amefanya mambo mengi yaliyowagusa walimu na kuwapa ari ya kufanya kazi.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja zaidi ya walimu 27,000 kwa awamu pamoja na 12,000 wanaotarajiwa kuajiriwa wataongeza idadi ya walimu na hivyo kuwapunguzia walimu vipindi na kuwawezesha kujiandaa vyema katika kufudisha wanafunzi vizuri.

Amesema kupitia kujengwa kwa vyumba vya madarasa zaidi ya 15,000 wanafunzi hawasongamani madarasani na hivyo kuwafanya walimu kuongeza tija katika kufundisha wanafunzi.

Hata hivyo amesema kuwa wapo baadhi ya walimu waliokuwa na madai sugu lakini Serikali imelipa madai hayo na bado inaendelea kulipa.

“Pia tumefarijika kwa ahadi ya Rais Samia ya kuongeza mishahara kwa watumishi ambao miongoni mwao ni walimu kwa hiyo suala la mishahara mipya tunalisubiri kwa hamu maana tunajua lipo katika hatua za utekelezaji.”

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif amesema wao ndio waliopeleka mapendekezo Serikalini ya ajira kutokana na mwitikio wa jamii katika kujitokeza kuandikisha watoto, na pia kutokana na walimu wanaofariki na waliostaafu.

Send this to a friend