
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema mashindano ya Ngao ya Jamii yatahusisha mechi moja ya Yanga na Simba itakayochezwa Septemba 16, 2025 mkoani Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na TFF imesema mfumo wa mashindano ya Ngao ya Jamii umebadilika kutokanana na marekebisho ya kanuni yaliyopitishwa katika kikao kilichopita cha Kamati ya Utendaji ya TFF.
“Moja ya marekebisho yaliyofanyika ni katika kanuni ambapo ikitokea mazingira kama ya sasa ambapo mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yamebana ratiba za TFF, itachezwa mechi moja tu ya Ngao ya Jamii badala ya tatu ambapo huanzia na nusu fainali mbili na kumalizia na fainali,” imesema TFF.
Tanzania ni mwenyeji wa Fainali za CHAN zilizoanza Agosti 2, 2025 na zitamalizika Agosti 30, 2025. Pia mwanzoni mwa Septemba TFF imesema timu ya Taifa (Taifa Stars) itacheza mechi mbili za Kombe la Dunia, na baada ya Ngao ya Jamii, klabu za Tanzania zitacheza mechi za raundi ya awali ya mashindano ya CAF.








