Dada wa kazi aliyemjeruhi kooni mtoto wa bosi ashikiliwa na polisi

0
64

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linamshikilia Clemensia Mirembe (19) ambaye ni Dada wa kazi za nyumbani kwa kosa la kumjeruhi na kitu chenye ncha kali mtoto wa mwajiri wake, Maliki Hashimu (6) Mkazi wa Goba Jijini Dar es salaam Julai 15, mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amesema mtuhumiwa anadaiwa kumkata na kitu chenye ncha kali eneo la shingoni, kilichotenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti na kumsababishia kushindwa kupumua, kuongea kupata pamoja na kupoteza damu nyingi.

Ameongeza kuwa mtoto huyo alipelekwa Hospitali ya Mloganzila na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mpaka sasa anaendelea kupatiwa matibabu.

“Baada ya tukio hilo la kikatili kufanywa na mtuhumiwa huyo, Jeshi laPolisi lilifanya jitihada kubwa za ufuatiliaji na baadaye Julai 21, 2024, mtuhumiwa huyu amekamatwa maeneo ya Goba akiwa amejificha kwenye jengo au jumba ambalo halijaisha,” ameeleza.

Muliro amesema mtuhumiwa huyo anahojiwa kwa kina, na atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.