Daktari jela miaka 200 kwa kukutwa na makosa 60

0
29

Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imemhukumu aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mlowo, Semeni Mswima kifungo cha miaka 200 jela au kulipa faini ya shilingi milioni 52.

Aidha, mahakama imemwamuru Mswima kurejesha shilingi milioni 30.9 alizoiibia Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.

Msimwa alikuwa akikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi Na.01/2021 iliyofunguliwa na TAKUKURU ambapo alikuwa akikabiliwa na makosa 60 yakiwemo makosa ya kutumia nyaraka za uongo kinyume na kifungu cha 342 na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya mwaka 2019 na makosa ya wizi kwa mtumishi wa umma kinyume na vifungu vya 258(1) na 270 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya Mwaka 2019.

Akisoma mashitaka hayo, Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa katika tarehe tofauti kati ya Julai 4, 2019 na Mei 8, 2020 kwa kutumia hati za malipo na hundi zilizoghushiwa aliweza kutoa na kuiba fedha jumla ya shilingi 30.9 kutoka katika akaunti Na. 61210014674 ambazo ni mali ya Halmshauri ya Wilaya ya Mbozi.

Mshtakiwa alikiri makosa yote 60 yaliyokuwa yakimkabili.

Hakimu Vitalis Changwe alimwamuru mshitakiwa kulipa faini ya shilingi 800,000 au kwenda jela miaka mitatu kwa kila kosa la kuwasilisha nyaraka za uongo, ambapo kulikuwa na jumla ya makosa 40.

Hakimu huyo pia alimwamuru mshitakiwa alipe faini ya shilingi 1,000,000 au kwenda jela miaka minne kwa kila kosa la wizi kwa mtumishi wa umma ambapo kulikuwa na jumla ya makosa 20.

Mshitakiwa alishindwa kulipa fedha hizo.

Send this to a friend