Daktari Nasriya Ali kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke amesema moja ya makosa yanayofanyika na kuchochea matatizo ya meno ni kusukutua baada ya kupiga mswaki, kwani kusukutua kunasababisha kuondoka kwa madini yaliyopo katika dawa ya mswaki ambayo yalitakiwa kubaki kwa ajili ya kulinda meno.
Daktari ameshauri kuzingatia aina ya dawa inayopaswa kuwa na madini ya floride ambayo yanazuia meno kutoboka na kufanya meno kuwa imara, hivyo unaposukutua madini yanayopatikana kwenye dawa hizo huondoka na meno kushindwa kuwa imara.
“Upigaji mswaki ni mazoea rahisi lakini muhimu kwa afya ya kinywa na mwili kwa ujumla. Kwa kufuata njia sahihi na kujali afya yako ya kinywa, unaweza kuhakikisha una kinywa kizuri na chenye afya kwa maisha yako yote,” ameeleza.
Mambo 6 hatari unayoyafanya kila siku
Aidha, amesema unatakiwa kupiga mswaki kwa muda usiopungua dakika mbili, mara mbili kwa siku, yaani baada ya kunywa chai asubuhi ili kuzuia mabaki ya chakula yasiwepo kwenye kinywa muda mrefu na kabla ya kulala.
Mbali na hivyo, Dkt. Ali amesisitiza umuhimu wa kutembelea daktari wa meno kwa ukaguzi na uchunguzi wa kawaida angalau mara mbili kwa mwaka ili kuweza kugundua matatizo yoyote na kuchukua hatua mapema.