Daktari mbaroni kwa kumbaka mtoto mgonjwa

0
56

Daktari Is-haka Rashid (35) mkazi wa Kangagani Wilaya ya Wete anayehudumu katika kutuo cha afya mjini Chake Chake, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa tuhuma za kumtorosha na kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 16.

Inadaiwa kuwa mtoto huyo alifika katika kituo hicho cha Afya Aprili 21 mwaka huu kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma, Daktari alimuomba namba yake ya simu ambapo aliwasiliana naye kwa ujumbe mfupi alipofika nyumbani kwa lengo la kufuata dawa ambazo hakuzipata kwa wakati ule.

Mtuhumiwa alimfuata binti huyo huku akijua kuwa anakwenda kuchukua dawa na badala yake alimpeleka nyumbani kwake kisha kumpima virusi vya Ukimwi na kuishi naye kwa siku tano huku akimbaka.

“Usiwe na wasiwasi wewe uko salama na mimi niko salama, hatuna maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kisha aliniletea futari na kupika. Alinambia simu niizime lakini siku ya tano baada ya kuwasha alinipigia shoga yangu na kunambia wazazi wangu wananitafuta” alidai

Mama wa binti huyo alidai, mwanaye aliaga kwenda shule lakini hakurudi ndipo walipo ripoti polisi, na siku ya tano aliongea naye kwa simu na kumsihi arudi nyumbani na mara aliporudi walimpeleka polisi moja kwa moja kwa ajili ya mahojiano na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Sadi Khamis, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa upelelezi utakapo kamilika atatoa taarifa.

Send this to a friend