Dar es salaam Jiji la sita kwa usafi Afrika
Rais Samia Suluhu Hassan amesema Jiji la Dar es Salaam limetangazwa na jarida la African Tour Magazine kuwa jiji la sita kwa usafi barani Afrika.
Amesema hayo wakati akishiriki maadhimisho ya Mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu Katoliki, Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
“Tumetoka mbali, kwa wale wanaoikumbuka Tanzania miaka kidogo ya nyuma, tulikuwa tunavijibanda na vimwamvuli kila pahali kwenye street [kwenye mtaa],” amesema Rais Samia akipongeza wote waliowezesha kuifanya Dar es Salaam kuwa safi.
Rais Samia ameongeza kuwa “Kwa sababu ya kutekeleza malengo hayo tuliyoelekezwa na Umoja wa Afrika na dunia, tumeweza kuisafisha Dar es salaam, na vivyohivyo tunasafisha majiji mengine makubwa kama Mwanza, Mbeya, Dodoma pamoja na Arusha,” amesema.
Aidha, amewapongeza viongozi wa dini kwa juhudi zao za utunzaji mazingira kwa kulinda vyanzo, misitu na upandaji miti, na kuwasihi viongozi kuzungumza na waumini wao ili kuthamini utunzaji wa mazingira katika jamii.
Ameongeza kuwa baadhi ya magonjwa yamekuwa yakizuka kwenye jamii kutokana na uharibifu wa misitu unaochangia viumbe vya misituni kuondoka kwenye makazi yao na kusambaa kwa watu.