DAR: Wafanyabiashara 45,000 wamefunga biashara na kugeuka Machinga

0
84

Wakati serikali ikiwa katika harakati za kutenga maeneo maalum na kuwahamishia wafanyabiashara wadogo, maarufu Machinga kwenye maeneo hayo, imeelezwa kuwa zaidi ya wafanyabiashara 45,000 katika mkoa wa Dar es Salaam pekee walifunga biashara zao, na kutoka kwenye mfumo rasmi wa biashara, kisha wakaanza kuuza bidhaa kama machinga.

Takwimu hizo zimetolewa na Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge wakati akitoa salamu katika hafla ya uzinduzi wa kuwapanga wafanyabiashara wadogo katika mkoa huo, ili kuondoa adha zinazotokana na ufanyaji wa biashara hovyo.

Mnyonge amesema katika kipindi cha miaka mitano au sita iliyopita wimbi kubwa la wafanyabiashara walifunga biashara zao na kuhamia kwenye umachinga, ambapo kwa kipindi hicho Manispaa ya Kinondoni ilikuwa ikipokea taarifa 150 kwa mwezi za kufungwa biashara, hivyo kufanya jumla ya wafanyabiashara 9,000 hadi sasa.

“Lakini nimewauliza na mameya wenzangu wa manispaa nyingine, hali ni hiyo hiyo kama inavyotokea Kinondoni. Kwa hiyo tulikuwa tunajaribu kuchukua takwimu za kihesabu kwa mkoa mzima, mpaka kufikia sasa ni zaidi ya wafanyabiashara 45,000 waliokuwa kwenye mfumo rasmi wamebadilika na kuwa wamachinga,” amesema Mnyonge.

Aidha, amesema Dar es Salaam kuna biashara ya watu ambao wanachukuliwa kutoka mikoa mingine na kufanishwa shughuli za kibiashara kwa kupewa meza, hivyo wanaonekana kama wao ndio wamiliki wa biashara, hivyo kuikosesha serikali mapato.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kizungumza ametoa mwezi mmoja wa maandalizi kwa kila wilaya kutenga maeneo ya kwa ajili ya wafanyabiashara hao, huku akitaja makundi ya wamachinga watakaoanza kuondolewa kuwa ni wale wanaofanya biashara kwenye hifadhi za barabara.

Wengine ni waliojenga vibanda juu ya mfereji/mtaro, wanaofanya biashara mbele ya maduka ya watu na kuzuia wateja kuingua na kutoka, kwenye njia za wanaenda kwa miguu na mbele ya taasisi za umma.

Makalla amesisitiza kuwa ufanyaji biashara hovyo unasababisha ajali, wizi, msongamano wa magari, kuzuia biashara za watu wengine na hatari za kimaisha kwani wapo wanaofanya biashara hadi chini ya tansfoma za umeme.

Send this to a friend