DAR: Wanafunzi wachorwa ‘tattoo’ kwa vitu vyenye ncha kali

0
37

Wanafunzi zaidi ya 30 wa Shule ya Msingi Mtongani, Kata ya Kunduchi mkoani Dar es Salaam wanadaiwa kuchorwa alama ‘tattoo’ mabegani na kitu chenye ncha kali.

Wanafunzi hao wanaoelezwa kuwa ni wa darasa la tano, sita na darasa la saba wamechorwa alama hizo kwa nyakati tofauti hivi karibuni.

Awali, taarifa za tukio hilo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa wanafunzi hao wamechorwa na mwanafunzi mwenzao anayedaiwa kutumwa na dada wa kazi.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, wanafunzi hao wamefikishwa katika Zahanati ya Kunduchi kwa ajili ya uchunguzi endapo alama hizo zimewasababishia madhara yoyoye ya kiafya.

“Ni kweli wanafunzi walikuja hapa kupimwa afya, na kwa vile maadili yanatuzuia kutoa taarifa hivyo nendeni shuleni,” amesema mmoja wa wahudumu wa zahanati hiyo.

Hata hivyo ripoti ya gazeti hilo imesema katika mazungumzo na wanafunzi shuleni hapo, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo amedai kuwa wanafunzi hao wamejichora herufi za majina yao kwa vijiti walivyochonga hadi kuwa na ncha kali.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amesema suala hilo wanaoweza kulizungumzia ni ofisa elimu hivyo wao walifika kusaidia mamlaka zingine na kuhakikisha hali ya utulivu inatawala.

Send this to a friend