Dar yaongoza kwa idadi ya wanaong’atwa na mbwa

0
57

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Arbogast Warioba amesema zaidi ya watu 20,000 wameripotiwa kung’atwa na mbwa kati ya Januari hadi Agosti mwaka huu huku mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza.

Ameyasema hayo Mpwapwa mkoani Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa duniani ambapo amebainisha mikoa inayoongoza kwa matukio hayo kuwa ni Dar es Salaam (3,321), Dodoma (3,136), Morogoro (1,559) na Arusha (1,155) ambapo idadi hiyo ni kwa wananchi waliopatiwa huduma katika vituo vya afya.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma ili kurahisisha huduma za chanjo kwa wanyama hususan mbwa na paka ili kuzuia ugonjwa huo ambao asilimia kubwa ya waathirika ni watoto wenye umri chini ya miaka 15.

Warioba amebainisha kuwa ugonjwa huo unakadiriwa kusababisha takribani vifo 59,000 kwa mwaka duniani, na asilimia 36 ya vifo hivyo hutokea katika bara la Afrika.

Send this to a friend