Daraja la mita 300 kujengwa eneo la Jangwani, Dar es Salaam

0
16

Serikali kupitia Mfuko wa Barabara (Road fund) imesema ipo tayari kupitisha kiasi cha shilingi bilioni nne kwa ajili ya kumlipa mkandarasi atakaepatikana ili kuboresha miundombinu ya jangwani mara baada ya uhakiki wa makisio hayo kukamilika na kujiridhisha.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Bodi ya mfuko huo, Mwenyekiti wa Bodi Bw. Joseph Haule, amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha inatatua changamoto hiyo haraka kabla ya mvua za masika kuanza.


“Bodi imeona tatizo hili na tumeliona kama suala la dharura, ndio maana tumekuja hapa kujionea hali halisi ili kutafuta njia sahihi ya kutatua tatizo hili ambalo limekuwa kero kwa muda mrefu”, amesema Mwenyekiti wa Bodi.


Aidha, Bw. Haule amefafanua kuwa kweli tatizo ni kubwa, mfereji una kina kifupi na makalvati mawili makubwa yaliyopo hapo yameziba kabisa.
Ameongeza kuwa nia ya Bodi ni kuona wananchi na wasafirishaji wanatumia muindombinu hiyo wakati wote wa mvua na kiangazi.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, amesema kuwa Serikali kupitia Wizara yake imeandaa mkakati wa muda mrefu kuhusu miundombinu hiyo ambapo amesema kuwa kwa sasa wataalamu wanafanya usanifu wa kina kwa ajili ya kuja na suluhisho la kudumu ikiwemo ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 300.


Mwakalinga amefafanua kuwa aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa haraka ikiwemo kutoa mchanga ambao umetuama katika eneo hilo ili kuinusuru miundombinu hiyo.


Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Julius Ngusa, amethibitisha kuwa ofisi yake inaendelea kuhakikisha kuwa michanga inayotuama katika eneo hilo inatolewa kwa wakati ili kuruhusu magari kuweza kupita mara baada ya mvua kunyesha.
Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara

wametembelea eneo la Jangwani kujionea hali halisi ya miundombinu katika eneo hilo ambayo imekuwa ikiathiriwa na mvua na kusababisha kufunga mawasiliano ya watumiaji wa barabara ya Morogoro hususani eneo hilo kila mwaka.

Send this to a friend