Daraja la Tanzanite kufungwa kwa saa 36

0
27

Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam umetangaza kuwa utafunga Daraja la Tanzanite kwa saa 36 ili kupisha maboresho ya baadhi ya miundombinu kwenye daraja hilo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa daraja hilo litafungwa Aprili 23 kuanzia saa 12:00 alfajiri hadi Aprili 24 saa 12:00 jioni na kuwa katika muda wote wa maboresho vyombo vya moto na watembea kwa miguu hawataruhusiwa kupita.

Hata hivyo, mamlaka hiyo yenye dhamana ya kusimamia barabara na miundombinu yake haijaeleza ni maboresho gani yanayotarajiwa kufanyika kwenye daraja hilo la kipekee Afrika Mashariki.

TANROADS imewataka wananchi kutumia barabara mbadala kwa muda wote huo ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza, na kuwa wanaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza.

Rais Samia Suluhu Hassan alizindua daraja hilo lenye urefu wa 1.03km Machi 24 mwaka huu, ambapo lilianza kutumia rasmi Febriari 1 mwaka huu.