Daraja la Tanzanite na Barabara ya Kibaha kuwekewa tozo

0
87

Serikali imesema magari yanayopita katika Daraja la Tanzanite yataanza kulipia fedha kwa kuwa daraja hilo lina sifa za kutoza fedha.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali Bungeni Dodoma, amesema Serikali inaendelea kuboresha sekta ya uchukuzi nchini ili kufungua fursa za kiuchumi.

Mpango wa kuweka tozo kwenye daraja hilo na baadhi ya barabara unakuja wakati ambao wananchi wa Kigamboni wanaendelea kuishinikiza serikali kuondoa tozo kwenye Daraja la Nyerere.

Mbali na Daraja la Tanzanite lenye urefu wa kilomita 1.03, barabara nyingine zitakazokuwa na sifa ya kuwekewa tozo ni pamoja na Kibaha- Mlandizi- Chalinze- Morogoro ambayo ujenzi wake ukikamilika utakuwa na urefu wa kilometa 158, pamoja na barabara ya Igawa- Songwe- Tunduma ambayo ikikamilika ujenzi wake itakuwa na urefu wa kilometa 218.

Katika bajeti hiyo serikali imesema itaweka msisitizo katika ujenzi wa barabara za kufungua fursa za kiuchumi na zile za kuunganisha Tanzania na nchi jirani.