Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umesema kuwa ujenzi wa daraja katika Mtaa wa Msumi, wilayani Ubungo, Dar es Salaam ambalo limelalamikiwa na wananchi kwa kuwasababishia adha kubwa ya usafiri litaanza kujengwa Agosti mwaka huu.
Taarifa ya TARURA imekuja baada malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo kuwasiliana na Swahili Times na kueleza adha wanayopata ambapo alisema daraja hilo liliharibiwa na mvua za El Nino tangu Oktoba 2023, na kwamba wamewasilisha malalamiko yao kwa mamlaka husika lakini hadi sasa hakuna matengenezo yaliyofanyika.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo alikwenda mbali na kueleza kuwa “sisi wananchi tumempigia kelele Mbunge Jumanne Mtevu, hajafanya lolote hadi sasa, zaidi ya kusema tusubiri mradi wa DMDP tangu mwaka jana, halafu mwaka huu tena akasema mradi utaanza mwaka mpya wa bajeti 2024/ 2025, mpaka sasa hakuna dalili ya chochote”.
Kufuatia malalamiko hayo, Swahili Times ilichukua jukumu la kuitafuta ofisi ya TARURA mkoa wa Dar es Salaam ambapo Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Geoffrey Mkinga amesema ujenzi wa daraja hilo unatarajia kuanza Agosti mwaka huu baada ya mkataba kusainiwa.
“Mkakati wa mwanzo ulikuwa ni kuwafanya watu waweze kuvuka lakini kwakuwa daraja lililokuwepo mwanzo liliondoka, ulitakiwa ufanyike usanifu upatikane ujenzi wa daraja kubwa-zuri, bahati nzuri ni kwamba eneo hilo lilikuwepo kwenye mradi wa DMDP awamu ya pili ambapo tayari tumekwishafanya usanifu wa kujenga daraja jipya,” ameeleza.
Kuhusu wananchi kudai walichanga pesa kwa ajili ya kuchukuwa jukumu la kufanya maboresho ya daraja lakini wakanyimwa kibali kutoka TARURA, Mkinga amesema hakuna pesa ambayo wananchi wanaweza kuchanga kutosha kujenga daraja kutokana na ukubwa wa daraja hilo.
“Hakuna hela ambayo wananchi pale wanaweza wakachanga ya kutosha kujenga pale, lile daraja ni zaidi ya milioni 500 linakimbilia kwenye milioni 800,” ameeleza.
Kwa upande wa Mbunge Msemvu amesema barabara tatu kubwa za zaidi ya kilomita 30 ndani ya jimbo hilo tayari ziko katika hatua za kuchakata mikataba na mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami ikiwemo barabara ya Msumi inayopita kwenye daraja hilo.
Amewasihi “wananchi waendelee sana kuwa wavumilivu, hayo mambo ya miradi mikubwa yanataka subira, mbunge wao nipo na napambania maendeleo ya jimbo langu.”