DART yapendekeza nauli kuwa TZS 1,500
Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) umependekeza nauli kwa njia jumuishi kuwa TZS 1,500 kutoka TZS 800 inayotozwa hivi sasa.
DART imetoa mapendekezo hayo katika kipindi hiki ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) ikitarajia kufanya mabadiliko ya nauli kwa mabasi hayo yaendeyo haraka maarufu mwendokasi.
Kwa mujibu wa taarifa ya LATRA, wameitisha mkutano wa wadau kutoa maoni ya nauli ya mabasi hayo baada ya kupokea maombi ya kurejea nauli za mabasi hayo kwa mkoa wa Dar es Salaam kutoka DART.
Katika mapendekezo yake DART inataka njia kuu ambazo abiria wanatozwa TZS 650 kwa sasa ipandishwe hadi TZS 1,200 na kwa njia ambazo abiria wanatozwa TZS 400 kwa sasa ipande hadi kufikia TZS 600.
Kwa upande wa njia jumuishi ambazo nauli TZS 800, DART imependekeza abiria watozwe TZS 1,500 na kwa wanafuzi wanaotozwa TZS 200 imependekezwa walipe TZS 300.