Dawa za steroids zimetengenezwa na binadamu na hutumika kutibu matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na matatizo ya homoni kama vile kuchelewa kubalehe. Dawa hizo pia hutibu matatizo ya misuli yanayotokana na magonjwa kama sararati na UKIMWI.
Hata hivyo baadhi ya wanamichezo na wabeba vyuma (body builders) huzitumia vibaya dawa hizo ili ziwasaidie kuwapa nguvu zaidi na kuboresha muonekano wao kwa kutunisha misuli.
Wengi wa wanaotumia dawa hizi ni wanaume wanaotaka kuwa na maumbile ya kuvutia. Baadhi humeza vidonge na wengine hujidunga sindano kwenye misuli au hupaka kama mafuta ambapo matumizi yao huwa kati ya mara 10 hadi 100 zaidi ya matumizi yanayotolewa na wataalam kwa wenye uhitaji.
Madhara ya matumizi ya dawa hizi kwa wanaume ni pamoja na kusinyaa kwa korodani, kupungua kwa kiwango cha mbegu za kiume, kipara, kukua kwa maziwa, huongeza hatari ya tezi dume.
Kwa wanawake madhara ni pamoja na kukua kwa nywele mwili (usoni), maziwa (matiti) kupungua, kipara, kubadilika au kukoma kwa mzunguko wa hedhi, mabadiliko sehemu za siri na kuwa na sauti nene.
Madhara yanayoweza kupata jinsia zote ni pamoja na chunusi, mikono na miguu kuvimba, matatizo ya figo na ini, moyo kutanuka, shinikizo la juu la damu, kujikweka katika mazingira ya kupata kiharusi, shambulio la moyo hata katika umri mdogo na hatari ya damu kuganda (mabonge mabonge).
Unashauriwa kupata ushauri wa mtaalamu wa afya endapo unasumbuliwa na tatizo lolote kati ya haya, na kuepuka matumizi ya hovyo ya dawa mbalimbali.