Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola imefanikisha kukamata jumla ya kilogramu milioni 1.96 za dawa za kulevya zikihusisha watuhumiwa 10,522 (wanaume 9,701 na wanawake 821) mwaka 2023.
Katika taarifa ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema dawa za kulevya zilizokamatwa ni heroin kilogramu 1,314.28, cocaine kilogramu 3.04, methamphetamine kilogramu 2,410.82, bangi kilogramu 1,758,453.58, mirungi kilogramu 202,737.51, skanka kilogramu 423.54 na dawa tiba zenye asili ya kulevya gramu 1,956.9 na mililita 61,672.
“Kiasi hiki cha dawa za kulevya kilogramu 1,965,340.52 zilizokamatwa katika kipindi cha Januari – Desemba 2023, ni karibu mara tatu ya kiasi cha dawa za kulevya zilizokamatwa nchini kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ambacho ni kilogramu 660,465.4,” imeeleza taarifa.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa dawa ngeni zilizoanza kuingizwa nchini hivi karibuni kama vile methamphetamine, skanka na biskuti zilizochanganywa na bangi pia zilikamatwa katika kipindi hicho.
Katika kuhakikisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanaimarishwa nchini, Serikali imesema imenunua boti yenye mwendo kasi ambayo pamoja na shughuli zingine itakuwa ikifanya doria baharini ili kufuatilia vyombo vinavyohisiwa kuingiza dawa za kulevya nchini kama vile Heroine, Methamphetamine na nyingine.