Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amevunja ndoa ya kimila iliyokuwa imefungwa kinyemela baina ya kijana mmoja ajulikanaye kama ‘Muddy Muuza Urembo’ wa Tunduru Mjini na msichana aliyechaguliwa kujiunga na elimu ya kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Masasi.
Mtatiro akishirikiana na vyombo vya usalama wamefanikiwa kuwakamata wazazi waliomuoza binti huyo pamoja na washenga waliohusika na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo majira ya saa 6 usiku akiwa anaishi na binti huyo wa shule kinyumba kwenye Kijiji cha Muungano, Tunduru Mjini.
Mzazi wa binti amekiri kumuoza binti huyo kwa mahari ya TZS 30,000 kwa madai kuwa binti hakuwa tayari kuendelea na kidato cha tano, huku binti akikiri kwa DC kwamba anapenda kuendelea na masomo yake ikiwa atapewa nafasi hiyo.
Binti amekabidhiwa katika taasisi inayolea na kufadhili mamia ya wanafunzi wilayani Tunduru ili kuhakikisha anaendelea na masomo yake.