Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imefanikiwa kukamata jumla ya tani 54.5 za dawa za kulevya za mashambani na viwandani pamoja na kuteketeza ekari 262 za mashamba ya bangi.
Dawa zilizokamatwa ni pamoja na bangi tani 54.48, mirungi kilogramu 10.3, heroin gramu 90.93, cocaine gramu 1.98 na kilogramu 4.623 za aina mpya ya dawa ya kulevya inayoitwa methylene dioxy pyrovalerone (MDPV) iliyokamatwa jijini Dar es Salaam ikisafirishwa na raia wa Comoro anayeitwa Ahmed Bakar Abdou (32).
DCEA imesema watuhumiwa 72 wamekamatwa kuhusika na dawa hizo na baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani.
“Methylene dioxy pyrovalerone (MDPV) ni dawa mpya ya kulevya iliyo katika kundi la vichangamshi inayotengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu. Dawa hii ina kemikali inayoweza kuleta madhara ya haraka kwa mtumiaji ikilinganishwa na dawa nyingine za kulevya. Pia, imeongezwa nguvu ya kilevi inayozidi cocaine, heroin na methamphetamine,” imeeleza taarifa ya DCEA.
Aidha, imesema dawa hiyo ya kulevya huuzwa kwa njia ya mtandao na husafirishwa kupitia kampuni za usafirishaji vifurushi na hufichwa kwa kuwekwa chapa za majina bandia kama vile bath salts, Ivory Wave, plant fertilizer, Vanilla Sky, na Energy.
Hata hivyo, DCEA imesema imebaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi katika hifadhi za misitu ya Ubangu mkoani Shinyanga na Mabatini mkoani Tabora ambapo wahalifu hao wamekata miti katikati ya misitu hiyo na kulima bangi hivyo kwa ushirikiano wa TFS walifanikiwa kuteketeza mashamba hayo na kuwakamata wahusika.