Denmark yasitisha mpango wa kufunga ubalozi wake nchini

0
17

Serikali ya Denmark imebatilisha uamuzi wa kufunga ubalozi wake nchini Tanzania ifikapo mwaka 2024.

Katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, uamuzi huo umekuja kufuatia mkutano wa 20 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika mjini Algiers, Algeria mwezi uliopita ambao ulihusisha nchi tano za Nordic ikiwemo Denmark.

“Mapema leo mwenzangu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Løkke Rasmussen, amenifahamisha kuwa serikali ya Denmark inabatilisha uamuzi wake wa kufunga ubalozi wake nchini Tanzania. Kwa hivyo, Denmark itaendelea na historia ya uwepo wake wa miaka 60 nchini Tanzania. Nimepokea habari hii kwa furaha, nikifahamu maana ya uhusiano kati ya nchi zetu mbili,” amesema Makamba.

Denmark ilitangaza uamuzi wa kufunga ubalozi wake nchini Agosti 27, 2021 na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Jeppe Kofod huku sababu zikielezwa kuwa ni kuendana na mpango wa nchi hiyo katika masuala ya kimataifa pamoja na vipaumbele vipya Serikali ya Denmark kwenye ushirikiano wa maendeleo.

Send this to a friend