Dereva asinzia na kusababisha ajali iliyoua watu 6

0
90

Watu sita wamefariki dunia hapo hapo na wengine wawili wamejeruhiwa baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso katika eneo la Runzewe wilaya ya Bukombe mkoani Geita leo alfajiri.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Safia Jongo amesema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Toyota Haice ikitokea Kahama kwenda Ngara na lori lililokuwa linatoka Rwanda kwenda Nairobi, Kenya.

Ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo dereva wa Haice alikuwa amesinzia na kuhama njia hali iliyopeleka magari hayo kugongana uso kwa uso.

Kamanda Jongo ametumia nafasi hiyo kuwatahadharisha madereva wanaoendesha vyombo vya moto majira ya usiku kuchukua tahadhari ili kuweza kuepukana na ajali ambazo zinaacha simanzi na majonzi kwa familia na jamii kwa ujumla.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika kituo cha afya cha Runzewe na majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.