Serikali imeanza kukutana na wadau wa masuala ya sheria kuona uwezekano wa kuondoa dhamana kwa makosa ya ubakaji na ulawiti ikiwa ni njia ya kupunguza malalamiko na kuwalinda watoto na wanawake kutokana na vitendo vya ukatili.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Happy Msimbe katika kikao kiichowakutanisha wataalam na wadau wa sheria kutoka wizara, taasisi za Serikali kwa lengo la kutoa mapendekezo ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
“Sisi timu ya wataalamu tumekutana hapa kwa kusudi la kujadiliana na kuona uwezekano wa kuondoa dhamana katika makosa ya ulawiti na ubakaji ili iweze kusaidia kudhibiti vitendo hivyo” amesema.
Uganda yapinga sheria ya kufanya chanjo kuwa lazima
Aidha, ofisa kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Ignas Mwinuka amesema katika tafiti waliyofanya, baadhi ya watuhumiwa wa makosa ya ulawiti na ubakaji wamekuwa wanakimbia na kutoweka na wengine kuharibu ushahidi au kumalizana na wazazi au ndugu wa muathirika wanapokuwa nje kwa dhamana.
Amesema nia ya kukusudia kutokuwa na dhamana katika makosa hayo, wameangalia pia katika sheria mbalimbali zikiwemo sheria za Zanzibar ambazo zimeweka kosa la ulawiti kutokuwa na dhamana.