Diamond afuta picha zenye bendera ya ubaguzi

0
71

Mwanamuziki Diamond Platnumz amefuta picha alizoweka kwenye ukurasa wake wa Twitter baada ya kukosolewa vikali na watumiaji wa matandao huku kutokana na picha hizo hizo kuonesha bendera inayoibua kumbukizi za ubaguzi wa rangi nchini Marekani.

Diamond ameweka picha hizo mapema leo asubuhi kama sehemu ya kuutangaza zaidi wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la Gidi, lakini bendera hiyo imeibua mjadala mkali hadi kupelekea mwanamuziki huyo kufuta chapisho lake.

Picha za Diamond zilikuwa na ‘confederate flag’ ambayo ilitumiwa na majimbo 11 ya Marekani yaliyotaka kujitenga miaka ya 1860 yakipinga kukomeshwa kwa biashara ya utumwa kwa sababu kwa sehemu kubwa yalitegemea watumwa kutoka Afrika katika shughuli za kilimo na uzalishaji mali.

Majimbo hayo ni Carolina Kusini, Mississippi, Florida, Alabama, Georgia, Louisiana, Texas, Virginia, Arkansas, Tennessee na Carolina Kaskazini.

Abraham Lincoln alipochaguliwa kuwa Rais wa Marekani, aliagiza utumwa usiendelee kuenea kwenye maeneo mapya, lakini wamiliki wa watumwa kutoka Kusini walihofia kwamba watumwa wao wanaweza kuwa ajenda inayofuata, hivyo wakaona njia pekee ni kujitenga.

Hata hivyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, majimbo ya Kusini yaliyokuwa yameenea katika shughuli za utumwa yalishindwa.

Mbali na kushinikiza utumwa, majimbo hayo yalitumia majukwaa yasiyo rasmi kueleza kwamba mtu mweupe ni mwenye hadhi kuliko mtu mweusi, na kwamba hilo ni jambo la kiasili.

Haya hivyo, baadhi ya watu wamesema kwamba Diamond kutumia bendera hiyo ni kuonesha kupinga ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi.

Send this to a friend