Dkt. Biteko aagiza kufumuliwa kwa kituo cha huduma kwa wateja TANESCO

0
31

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameagiza kufumuliwa kwa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO) kufuatia kituo hicho kushindwa kuwahudumia wananchi kwa viwango vinavyotarajiwa.

Ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea kituo hicho pamoja na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yake aliyoyatoa mwezi Aprili, 2024 ambapo amesema Serikali ya Rais Samia imetoa fedha nyingi kuhudumia kituo hicho lakini utendaji wake ni mbovu kuliko huduma ya kituo.

Dkt. Biteko ameshangazwa na hatua ya TANESCO kuweka kando maelekezo ya mwezi Aprili 2024 yaliyolitaka Shirika hilo kuondokana na matumizi ya namba za kulipia kwenye utoaji wa huduma na kuomba namba ya bure ya huduma (free toll number) kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kuwapa unafuu wananchi wanaohitaji huduma za TANESCO.

” Wewe ulishapiga simu, pesa yako ikakatwa na huduma usiipate? Wananchi wanaumia sana!” naagiza kuundwa upya kituo ili kuongeza ufanisi na tija kwa wananchi, “kituo hiki kinategemewa na Watanzania wengi na huduma inayotolewa hapa hairidhishi kabisa,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ametoa wiki moja kwa uogozi wa TANESCO kufanya maboresho ya kituo hicho, na matokeo yake yawe wazi kwa wananchi kutokana na huduma zake.

Akizungumzia utendaji wa Kituo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Abubakar Issa amesema kulikuwa na changamoto za kibajeti na kwamba Aidha kwa kushirikiana na TCRA watakaa haraka na kuanza matumizi ya namba bila malipo ili kutoa unafuu kwa wananchi na kuleta tija kwa watumiaji.