Dkt. Biteko asisitiza umuhimu wa uelimishaji matumizi ya nishati safi ya kupikia

0
6

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesisitiza umuhimu wa kampeni ya uelimishaji katika kufanikisha malengo ya kitaifa ya Nishati Safi ya Kupikia.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa Mkakati wa Mawasiliano wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Kampeni ya Uhamasishaji kuhusu nishati safi, hafla iliyofanyika jijini Dodom.

Uzinduzi huo ni hatua muhimu katika juhudi za taifa kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi kwa upishi ifikapo mwaka 2034, kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa kwenye Mkakati wa Taifa wa Upishi Safi 2024–2034.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka nishati safi kuwa kipaumbele cha kitaifa katika maendeleo. Uzinduzi huu wa Mkakati wa Mawasiliano na kampeni ya kitaifa unaonesha dhamira yetu ya kuwafikia Watanzania wote ili kuleta mabadiliko. Bila uelewa, hakuna mabadiliko. Kampeni hii ni wito kwa kaya, jamii, na taasisi kukumbatia matumizi ya nishati safi na ya kisasa,” amesema.

Akiendelea kufafanua juu ya dira ya kampeni hiyo, amesema kampeni ya uhamasishaji itatekelezwa kwa awamu ikianza na ujumbe kupitia vyombo vya habari kitaifa, ikifuatiwa na mikakati ya uhamasishaji katika jamii, elimu kupitia shule, na maonesho ya masoko.

“Lengo letu ni kujenga mazingira rafiki ambapo maarifa haya yatachangia kuleta mabadiliko ya tabia, na mabadiliko hayo kuleta mahitaji ya nishati safi. Hii ni safari ya miaka kumi inayoanza leo, na kila kata na kijiji kitakuwa sehemu ya kampeni hii. Tumejipanga kushirikisha viongozi katika ngazi zote ili ujumbe wa nishati safi uweze kuwafikia Watanzania wote,” ameongeza.

Kampeni ya kitaifa ya miaka kumi ya uhamasishaji itatumia njia mbalimbali za mawasiliano kuwafikia wananchi wengi nchini. Itajumuisha vyombo vya habari kama redio, televisheni, magazeti; itahusisha ushirikishwaji wa jamii kupitia matukio ya moja kwa moja, maonesho ya barabarani, na programu katika shule; pia itatumia majukwaa ya kidigitali ikiwemo mitandao ya kijamii, ujumbe mfupi wa simu (SMS), na programu za simu.

Aidha, kutakuwa na ushirikiano na viongozi wa dini, walimu, taasisi za kijamii, na watu wenye ushawishi katika jamii. Mbinu hiyo shirikishi inalenga kuleta ushiriki wa kudumu wa wananchi, kubadili mitazamo, na kuongeza matumizi ya teknolojia za nishati safi majumbani na katika jamii.