Dkt. Gwajima: Hakuna ugonjwa wa ajabu Kata ya Ifumbo, Mbeya

0
50

Wizara ya afya imekanusha taarifa za uwepo wa ugonjwa usiofahamika wala janga lolote la kiafya katika Kata ya Ifumbo, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima amesema timu ya wataalamu iliyofika katika eneo hilo imebaini kuwa si kweli kwamba kuna vifo vya watu 15 kwa mara moja vya ugonjwa unaodaiwa kupelekea watu kutapika damu kama ilivyoripotiwa na Diwani wa Kata ya Ifumbo.

Dkt. Gwajima amesema kuwa pasi na kuwa na ushahidi na takwimu zilizotolewa, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya, Dkt. Felista Kisandu aliungana na diwani kwenye ajenda hiyo na hivyo kusababisha taharuki kwenye jamii bila sababu.

“Hata kama kungekuwa na mlipuko aina yoyote ile ni dhahiri kuwa Dkt. Kisandu alikiuka mwongozo wa utoaji wa taarifa za mlipuko kwani mwenye dhamana hiyo ni waziri wa afya baada ya kujirodhisha na siyo vinginevyo,” imeeleza taarifa hiyo.

Kufuatia hatua hiyo, waziri ameagiza kusimamishwa kazi mganga huyo ili kupisha uchunguzi, na ameagiza kupewa majibu ndani ya siku 10.

Aidha, amesema  wizara hiyo itachukua hatua ya kupeleka malalamiko au mashitaka wizara na vyombo vinavyohusika  na maaadili ya utoaji habari.

Waziri amewaasa wananchi kutumia taarifa za afya zinazotolewa na watu wenye dhamana na sio kila mwananchi awe msemaji kwenye masuala ya afya.

Send this to a friend