Katika mwezi huu wa Ramadhan familia nyingi nchini na duniani kwa jumla kuna nchi ambazo raia wake wanafunga saumu hii tukufu kama nguzo moja kati ya tano za kiislaam. Chakula cha jioni au kama kinavyojulikana IFTAR/FUTARI mbali ya kuwa na aina mbali mbali za vyakula bali pia huwa ni vingi kuliko siku za kawaida.
Kula futari nyingi kipindi cha Magharibi sio tu kutafanya wafungaji na waalikwa wengine kuongezeka uzito mwezi huu wa Ramadhan bali kwa wale walaji ambao wana matatizo mbalimbali ya moyo kama shinikizo la damu la juu (High Blood Pressure), moyo dhaifu (heart failure), moyo uliopanuka (Dilated Cardiomyopathy), mishipa/mirija ya moyo iliyoziba (coronary artery disease CAD) wanaweza kupata matatizo ya kiafya .
Ulaji wa chakula kingi kunaweza kuchochea mshtuko wa ghafla wa moyo (trigger heart attack). Mshtuko wa moyo unasababisha mamilioni ya watu kupoteza maisha kila mwaka duniani. Kila mwaka vifo hivi vinaongezeka zaidi duniani kipindi hiki cha Ramadhan na wakati wa sherehe mbalimbali kama vile Krismasi, Pasaka na Mwaka Mpya.
Kwanini vifo vinavyotokana na mshtuko wa moyo vinaongezeka kipindi cha Ramadhan?
Tafiti zinaonesha kipindi kama hiki cha Ramadhan vifo vinavyotokana na mshtuko wa moyo huongezeka mara nne (4) zaidi. Kuna sababu kadhaa zinazoweza sababisha kuchochea mstuko wa moyo. Sababu hizo ni;
- Unapokula chakula kingi mpaka kuvimbiwa wakati wa kufuturu/iftar au wakati wa daku, tumbo la chakula linapanuka ili kupokea chakula hicho hii itapelekea damu mwilini kujipanga upya kwa kutoa damu nyingi kutoka kwenye moyo kuelekea/ kupelekwa “redistribution” kwenye njia ya chakula “Digestive System” ili kusaidia kumeng’enya “digest” chakula kingi kilicholiwa nyakati za futari/daku. Hali hii ikimkuta mlaji ambaye ana tatizo la moyo au shinikizo la damu la siku nyingi/zamani (kwa mfano mirija au mishipa yake ya damu ya moyo imeziba kidogo au sana) huu mbadiliko wa mwendo wa damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye tumbo ndio unapelekea kuchochea “trigger heart attack” ambayo itasababisha mshtuko wa moyo na athari zake.
- Tumbo lililojaa kutokana na ulaji wa chakula kingi sana husababisha moyo kwenda mbio “palpitation” na/au mapigo kutokwenda sawasawa “irregular heartbeats” hii pia huchochea mshtuko wa moyo na wengine kupata kiarusi “stroke”.
Ni muhimu Watanzania kufahamu kuwa;
- Magonjwa ya moyo yanaongoza duniani kusababisha vifo ukilinganisha na magonjwa mengine yeyote.
- Zaidi ya watu millioni 18 hufariki duniani kila mwaka kwa sababu ya magonjwa ya moyo, hii ni asilimia 31% ya vifo vyote duniani. Kati ya hivi vifo vya moyo asilimia 85% vinatokana na mshtuko wa moyo “heart attack”.
- Robo tatu (3/4) ya vifo hivi vya moyo vinatokea kwenye nchi zenye uchumi mdogo au uchumi wa kati (low/middle income countries).
- Asilimia kubwa > 80% ya magonjwa ya moyo yanaweza kukingika kwa mfano kuacha uvutaji wa sigara, kula vyakula bora na kwa kiasi (kumbuka bibi zetu walikuwa wanasema usile mpaka uvimbiwe), kupunguza uzito, kufanya mazoezi, kupunguza unywaji wa pombe nk.
- Wale waliogundulika na matatizo ya moyo, shinikizo la juu la damu, kisukari, uzito mkubwa “overweight na obesity” kufuata masharti ya madaktari wao. Ushauri:
- Ukiona dalili za tatizo la moyo kuchoka kuliko kawaida “fatigue”, shida ya kupumua sawa sawa, kiungulia/maumivu ya chembe “heartburn” na maumivu kifuani. Tafadhali tafuta kwa haraka ushauri wa daktari. Dalili hizi wakati mwingine haziwezi kuondoka zenyewe.
- Tufungue funga zetu au tule kwa kiasi hasa tule vyakula vyenye protein nyingi kuliko wanga mwingi na hili hasa kwa wale wenye matatizo ya moyo kabla ya mfungo au yamengundulika mwezi huu. Kupunguza vyakula vyenye sukari nyingi.
Ushauri huu wa ulaji wa chakula nimeutoa kwa kila Mtanzania.
Ramadhan Kareem.
Profesa Mohamed Janabi MD.,PhD.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili
(Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza Mei 2021)