Dkt. Kikwete: Mchakato wa kuhamia Dodoma ulikuwa wa kidemokrasia

0
43

Takribani miaka 50 baada ya kupitishwa kwa uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Tanzania, bado watu wengi hawakuwa wakifahamu namna mchakato mzima ulivyofanyika.

Akizungumza leo Mei 30, 2020 katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa ofisi za Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt Jakaya Kikwete amesema kuwa mchakato huo ulikuwa wa kidemokrasia.

Amefafanua kuwa, uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma halikuwa wazo la mtu mmoja, bali baada ya kuanza vuguvugu la kufanya katikati ya nchi kuwe ndio makao makuu, mikoa ilitakiwa kutoa maoni ambapo mingi ilikubaliana na pendekezo, huku michache ikipinga.

“Uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma, ulifanywa kidemokrasia. Mikoa ilitakiwa kuja kutoa maoni, mingi ilikubali, lakini mmoja wa mikoa iliyokataa ni Mkoa wa Pwani,” amesema Dkt. Kikwete

Akieleza sababu ya Pwani kukataa amesema kuwa, wazee hawakutaka serikali kuhamia Dodoma kwa sababu ni mbali na wao tayari walikuwa wamezoea Dar es Salaam.

Wakati huo huo, amesema kuwa Wajerumani walipokuja nchini uongozi ulikuwa Bagamoyo, lakini wakoloni hao walitaka sehemu yenye bandari ndio maana walihamia Dar es Salaam.

Send this to a friend